Tuesday, April 21, 2015

0
MSANII FEROOZ ATIWA MBARONI KWA UTAPELI

Mayasa Mariwata na Makongoro Ogin’g
Tena? Kwa mara nyingine staa wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho ametiwa mbaroni kwa utapeli akidaiwa ‘kuchikichia’ fedha za kumpangisha nyumba jamaa aliyejitambulisha kwa jina la Tony Noah kiasi cha zaidi ya Sh. milioni 3.2 kisha kuingia mitini ikielezwa kuwa nyumba hiyo ina mgogoro.
Staa wa Bongo Fleva, Ferooz Mrisho.
Kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika, ilidaiwa kwamba, staa huyo aliyewahi kutamba na Ngoma ya Starehe amekuwa na tabia ya kuwaingiza watu mkenge kwa lengo la kutafuta mpangaji kwenye nyumba hiyo iliyopo Sinza- Mori, Dar ambayo anaishi na ndugu zake.
Kilitiririka kuwa, awali Ferooz alikuwa akitafuta mpangaji wa nyumba hiyo kupitia kwa dalali ndipo Tony akavutiwa na nyumba hiyo na kukubaliana kutoa kodi ya Sh. milioni 3, 250,000 kwa mwaka.Kilidai kwamba Tony alipomlipa Ferooz fedha hiyo, Machi 14, mwaka huu ndipo akaanza kumpiga kalenda ndipo aliamua kulipeleka shauri kwenye chombo cha sheria.
Kutokana na sekeseke hilo, mwanahabari wetu alimtafuta Tony ambaye alisema kuwa, baada ya kukubaliana na Ferooz kumpa fedha hizo na kuona anaanza kumzungusha kuhamia kwenye nyumba hiyo alimwambia waandikishiane kwenye Kituo cha Polisi Kijitonyama, Dar (Mabatini) kuwa atamlipa fedha hizo Aprili 15 lakini Ferooz hakufanya hivyo.
Kutokana na ishu hiyo, hadi gazeti hili linakwenda mtamboni, Ferooz alikuwa ameshikiliwa Mabatini kwa jalada la kesi namba KJN/RB/3898/15 KUJIPATIA FEDHA KWA NJIA YA UDANGANYIFU.Mwaka jana Ferooz alishikiliwa kituoni hapo kwa msala wa kukamatwa na bangi.

0
WATU 20 WAJITOKEZA KUGOMBEA UBUNGE JIMBO LA SEGEREA KUPITIA CHADEMA

Makada 20 wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameonyesha nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Segerea.

Mbali ya makada hao, watu wengine 50 wamejitokeza kuwania nafasi ya udiwani katika jimbo hilo.
Kwa sasa mbunge wa jimbo hilo ni Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Dk. Makongoro Mahanga aliyeshinda katika uchaguzi wa mwaka 2010 kwa kura 43,554 (asilimia 41.7) wakati mpinzani wake,Fred Mpendazoe alipata kura 39,150 .
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Segerea, Gango Kidero alisema lengo ni kutetea maslahi ya wananchi ndani ya jimbo hilo.
Alisema licha ya makada hao kuonyesha nia,uamuzi wa mwisho upo kwa viongozi wa juu wa chama hicho kupitisha jina la mgombea mmoja baada ya Chadema kuungana na vyama vingine vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi(Ukawa).
Tuna zaidi ya watu 70 walioonyesha nia ya kuwania ubunge na udiwani wa Jimbo la Segerea lengo ni kulichukua kutoka mikononi mwa Chama Cha Mapinduzi(CCM),” Kidero.
Alisema watangazania wote ni wasomi wazuri wenye fani mbalimbali na wamekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya wananchi ndani na nje ya jimbo hilo.

0
MCHUNGAJI ATANGAZA NIA YA KUGOMBEA URAIS KAMA MGOMBEA BINAFSI

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Stephano Moshi (SMUCCO), Mchungaji Godfrey Malisa, ametangaza nia ya kugombea urais Oktoba mwaka huu kwa tikeki ya mgombea binafsi.
Mchungaji Malisa, alitangaza azma hiyo huku Serikali ikiwa bado haijaweka bayana kuwepo kwa mgombea binafsi kwa sababu Katiba Inayopendekezwa haijapitishwa.
Mwaka 2010, Malisa aligombea ubunge Jimbo la Moshi kwa tiketi ya
Chama cha Tanzania Labour (TLP).
Alisema ameamua kuchukua uamuzi huo ili kurejesha heshim Julius Nyerere.a ya taifa, kama ilivyokuwa imejengwa na na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu.
Hata hivyo, alisema enzi za Mwalimu Nyerere lilikuwa na heshima kubwa ndani na nje ya nchi ambapo tangu kuondoka madarakani hajaweza kupatikana kiongozi wa kuvaa viatu vyake.
“Mimi nimeishi Marekani na China…taifa letu lilikuwa linaheshimika, leo hii hata amani imeanza kutoweka kutokana na maujai ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ujambazi na wizi wa fedha za umma,” alisema.

0
ASKARI AUGUA KICHAA...KILICHOFUATIA KIKO HAPA

SoldierHii nimekuta kwenye mtandao wa gazeti maarufu Uingereza, linaitwa The Independent.. wameandika ripoti inayoonesha kwamba kuna kundi kubwa sana la Wanajeshi wa Uingereza ambao wamegundulika kuumwa ugonjwa wa akili, sababu ya ugonjwa huo ni dawa ambazo huwa zinatumiwa na Wanajeshi hao ili kuzuia wasipate maambukizi ya Malaria !!
Dawa hizo zinaitwa Mefloquine au jina jingine Lariam.. tayari toka 2008 mpaka leo kuna wanajeshi karibu 1,000 ambao walipata matatizo ya akili kutokana na kutumia dawa hizo wakiwa nje ya Uingereza kupigana vita.
Athari nyingine baada ya kutumia dawa hizo ni pamoja na kupata stress, na wengine wanajiua kabisa!
Alastair Duncan ni Meja Jenerali Mstaafu wa Jeshi hilo ambae aliwahi kwenda kwenye vita Sierra Leone, yeye ni mmoja ya walioathirika kwa kupata tatizo la akili baada ya kutumia dawa hizo.

0
WAMUOMBA RAIS KIKWETE KUTOSAINI MUSWADA HUU WA SHERIA

Wasomi na wananchi mbalimbali, wamemuomba  Rais Jakaya Kikwete, kutosaini Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 huku wakieleza kuwa kama utasainiwa watahamasisha wananchi kuupinga kwa kufanya maandamano ya nchi nzima mitaani.
Aidha, wamesema muswada huo ukisainiwa watatumia kama fimbo kukiadhibu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kutokichagua katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba, mwaka huu.
Walisema hayo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mdahalo uliowashirikisha wananchi, wanafunzi mbalimbali wa vyuo vikuu na wahadhiri wa vyuo vikuu kujadili athari za Sheria ya Takwimu  ya mwaka 2015 na Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015.
Wakati wa Bunge la 19 lilohitimishwa Aprili Mosi, mwaka huu, miswada hiyo iliwasilishwa na serikali bungeni kwa hati ya dharura na kupitishwa na Bunge na sasa hatua inayofuata utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kuisaini ili iwe sheria ianze kutumika.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Prof. Kitilia Mkumbo, akizungumza katika mdahalo huo alisema miswada hiyo kama itasainiwa na Rais na kuwa sheria, itakuwa na athari kubwa kwa wahadhiri na wanafunzi wa vyuo vikuu.
Profesa Mkumbo alisema kwa mfano, Sheria ya Takwimu ikianza kutumika itarudisha nyuma kupata wanafunzi wa PhD kwa sababu masomo yao yanategemea sana kupata takwimu.
Usalama mkubwa kuliko wote ni uhuru wa kupata taarifa, kutokupata taarifa sahihi kuna hatari,” alisema.
Profesa Mkumbo alisema Watanzania wanapenda kulalamika tu vijiweni lakini hawachukui hatua na kwamba katika suala la muswada huu kuna haja kwa wananchi kuandamana mitaani ili Rais asisaini.
Ndigwa Ezekiel, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alieleza wasiwasi wake kama suala hilo likienda kupingwa mahakamani haki itatendeka kwa madai kuwa imeegemea upande wa serikali.
Wachangiaji wengine walisema kama miswada hiyo itasainiwa, hawataipigia kura CCM katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Wakati wa Mkutano wa Bunge, serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 na kueleza kuwa mtu akatayebainika kusambaza picha za ngono, miili ya watu waliokufa kwa ajali na usambazaji taarifa za siri za serikali, atatozwa faini ya Sh. milioni tano, kifungo kisichopungua miezi sita au vyote kwa pamoja.

0
MWANAMKE HUYU AOLEWA MARA MBILI....MUME WA PILI HAKUJUA KITU...!!!

Rings-on-FingersIshu ni kwamba kuna mwanaume alikutana na msichana wakapeana namba za simu wakawa wanawasiliana, wakaanzisha uhusiano, baadae wakafunga ndoa.. kilichoibuka baadae kumbe yule mwanamke ni mke wa mtu !!
Mwanaume huyo amesema alipokutana na mwanamke huyo alimwambia kuwa ni mwanafunzi  wa kidato cha tatu, wakaendelea na uhusiano hadi binti alipomueleza kuwa amemaliza shule na kujiunga VETA, akasoma mpaka akamaliza. uhusiano wao ulidumu kwa miaka miwili, hakuna tatizo lolote lilitokea hapo katikati.
Wakakubaliana waoane.. Mwanaume akapeleka barua ya posa kwa wazazi wake na harusi ikafungwa nyumbani kwao Zanzibar.
Wakiwa ukumbini wazazi wa mwanaume wakasikia tetesi kuwa mwanamke huyo ameolewa na ana familia yake.. wakaanza kufuatilia na kugundua kuwa mwanamke huyo ameolewa na ana watoto wanne, yuko kwenye ndoa kwa miaka 16.. ndoa hii mpya haikwenda mbali, ilivunjika ndani ya wiki moja.

0
LHRC yaitaka serikali kutoa machapisho ya kutosha ya katiba pendekezwa

Wakati taifa likielekea kuipigia kura katiba inayopendekezwa kumejitokeza changamoto  ya upatikanaji wa  katiba hiyo kutokana na kuwepo na machapisho machache ya katiba inayopendekezwa na hivyo kituo cha sheria na haki za binadamu(LHRC) kimeitaka serikali kuchapisha  machapisho ya kutosha ya katiba hiyo ili wananchi waweze kuisoma na kuielewa.
Hayo yameelezwa na mwanasheria wa kituo cha sheria na haki za binadamu (LHRC) Bi.Geline Fuko wakati akizungumza katika mikutano mbalimbali ya kutoa elimu kuhusiana na katiba inayopendekezwa  mjini songea.
 
Bi.Geline Fuko amesema katika maeneo mbalimbali waliyozunguka wamebaini kuwa  machapisho ya katiba  pendekezwa  yako machache hivyo wameitaka serikali  kuchapisha machapisho hayo ya kutosha.
 
Katika mkutano uliofanyika chuo cha ualimu Songea TTC na kuwashirikisha wanachuo na walimu katika chuo hicho wanachuo wamekosoa katiba pendekezwa  kutokidhi matakwa ya wananchi.

0
Jeshi la polisi linawashikilia watu watatu kwa makosa ya kuwakuta na karatasi 860 za dola bandia mkoani Ruvuma

Jeshi la polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu watatu akiwemo  mzambia mmoja kwa kukutwa na karatasi  nyeusi 860 za dola bandia za kimarekani zikiwa katika mafungu ya bunda kumi ambapo kila bunda lina karatasi themanini na sita huku pia wakiwa na malighafi ya kutengeneza dola hizo ambazo wakichanganya na karatasi hizo zinageuka kuwa dola bandia.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa ruvuma ACP MIHAYO MSIKHELA amewataja watuhumiwa wa tukio hilo kuwa ni Boniface   Simwanza mwenye miaka 41 raia wa zambia,Adamu Msongore mwenye miaka 26 mkazi wa tunduma mkoani mbeya na Hatman Steven mkazi wa makumbusho Songea huku pia wakiwa na malighafi za kutengeneza dola bandia.
 
Kamanda Msikhela amesema kuwa polisi inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na utakapokamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma za tukio hilo. 

Kufuatia tukio hilo jeshi la polisi mkoa wa Ruvuma linawataka wananchi hasa wafanyabiashara kuwa waangalifu na matapeli wanaotengeneza noti bandia 

0
Waziri Membe asema hakuna Mtanzania aliyeuawa AFRIKA KUSINI, 21 kurejea nchini


Watanzania 23 waishio Afrika Kusini wamewekwa kwenye kambi maalumu ya Isipingo nchini humo ili kupewa ulinzi wa maisha yao yaliyo hatarini kufuatia mashambulizi yanayofanywa na wazawa dhidi ya wageni. 
 
Watu hao ambao ndiyo idadi ya Watanzania waliotambulika kuwa hatarini nchini humo, wanatarajia kuwasili nchini muda wowote baada ya Serikali ya Afrika Kusini kuridhia.
 
Watakaorejea nchini ni Watanzania 21, wengine wawili wameomba kuendelea kubaki huko.
 
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha katika vurugu zilizosababishwa na chuki dhidi ya wageni, lakini wapo Watanzania watatu waliokufa nchini humo kwa sababu nyinginezo.
 
Membe aliwataja waliofariki kuwa ni Rashid Jumanne. Alisema Mtanzania huyu alikuwa ni jambazi na aliuawa kilomita 90 kutoka mji wa Durban akiwa kwenye harakati zake za unyang’anyi.
 
Mtu wa pili alisema anaitwa Athman China. Alisema kijana huyu aliuawa kwa kuchomwa kisu ndani ya gereza la West Hill. Membe alifafanua kuwa China alifanya kosa la jinai akafungwa, na huko gerezani zikatokea fujo za wafungwa. Kijana huyo alikufa baada ya kuchomwa kisu na wafungwa wenzake.
 
Ally Mohamed alikuwa ni kijana wa tatu kufa akiwa Afrika Kusini. Membe alisema Mohamed alikuwa amelazwa hospitali huko Johanesberg kwa maradhi ya kifua kikuu.
 
Kijana huyo alifariki baada ya kuugua kwa miezi miwili, na tayari mwili wake umewasili nchini kwa maziko.
 
“Kuna habari zimesambaa mitandaoni kwamba Watanzania wamekufa huko Afrika Kusini. Niweke wazi kuwa hakuna Mtanzania aliyepoteza maisha kutokana na vitendo vya chuki dhidi ya wageni.
  
Mpaka sasa ni watu nane tu ndiyo waliopoteza maisha,” alisema waziri huyo na kuongeza kuwa watu hao wanatoka katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Malawi na Swaziland.
 
Membe alisema aliwasiliana na Waziri wa Usalama wa Afrika Kusini, David Mahlobo akamthibitishia kuwa hakuna Mtanzania yoyote aliyekufa.
 
Pia, alimwita balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini ili aeleze zaidi madhara yaliyojitokeza kwa Watanzania waishio Afrika Kusini.

0
Kuna Taarifa za Muigizaji Wastara Juma kupata Ajali,Soma HapaMwigizaji Wastara leo ameandika maneno zaidi ya 100 na kuambatanisha na picha kuthibitisha kuhusu ajali aliyoipata japo hajaandika kwa undani zaidi kuhusu ajali yenyewe.
 
Wastara baada ya kuweka hii picha haya ndio maelezo aliyoyatoa :
 

"DUA ZENU MUHIMU SANA KWA MBAO MNAONIPENDA NA MSIONIPENDA……hali hii imenichosha sana ya matukio ya ajali kila mara natamani kuwa na amani na maisha yangu couz mungu ana sababu kuniacha niendelee kupumua mpaka leo
 
"Ila kwa wanaochukia kuona napumua wanatamani nizikwe hata mzima ila mtambue nina watoto watatu wananitegemea kwa kila kitu sometime mnasema nasikitika sana ni kweli sababu mi sio nabii nikihesabu hii ni ajali ya ya 9 sasa tena ni mbaya sana za kufa kabsa ila labda nimo kwa wale wanaopta ajali kipindi hiki japo kwangu ni too much,, ni jana na leo napumua alhamdulilah duwa zenu niombeni jamani huyu jinamizi akae mbali nami daah too much"

0
Lulu: Sina cha Kusema Wala Tamko Kuhusu Kifo cha Seki


Kufuatia kuhusishwa na kuwa na mahusiano ya kimapenzi na marehemu Bilionea Lusekelo Samson Mwandenga ‘Seki’ aliyefariki dunia Alhamisi iliyopita, Staa wa Bongo Movies Elizaberth Michael ‘Lulu’ amesema hana la kusema na hana tamko lolote fufuatia kifo cha Seki.

Akiongea na gazeti la Ijumaa Wikienda Juzi, lililotaka kujua taarifa za yeye kuhusishwa na bilionea huyo pamoja na mambo mengine, Lulu alijibu kwa kifupi;

Mwandishi: “Lulu kwanza tumesikia unaumwa na umelazwa, ni kweli?”

Lulu: “Siyo kweli, mimi mbona nipo tu hapa nyumbani.”

Mwandishi: “Kuna manenomaneno kuhusu kifo cha Seki, watu wanakusema vibaya mitandaoni. Je, unatoa tamko gani?”

Lulu: “Sina tamko lolote.”

Mwandishi: “Lakini ni mtu uliyekuwa unamfahamu au alikuwa mpenzi wako?”

Lulu: “Sina cha kusema mimi na sina tamko lolote.”

Alipobanwa kwa maswali zaidi kuhusiana kuwa na uhusiano na bilionea huyo, kutofanyika kwa bethidei yake na kufuta akaunti ya Instagram, Lulu hakuwa tayari kujibu lolote.

0
Diamond Akiri Kulifahamu Tatizo la Wema la Kutopata Mtoto Muda Mrefu, Adai Walijaribu Kulitafutia Tiba Lakini Hawakufanikiwa


Kwa muda mrefu, Diamond Platnumz alikuwa akilijua tatizo la mpenzi wake wa zamani Wema Sepetu la kutoshika mimba.

Akiongea na kipindi cha Ng’ari Ng’ari cha Clouds TV, Diamond alisema wakati wako pamoja waliwahi kuzunguka kwa wataalam mbalimbali kujaribu kupata tiba lakini hawakufanikiwa. Alisema ilifika wakati alimweleza tu kuwa akubali hali hiyo.

Kuhusu kile Wema alichokiandika kwenye Instagram hivi karibuni ambapo alieleza ukweli wa hali yake ya kutopata mtoto, Diamond alisema ujumbe huo ulimuumiza kama wengine walivyoumia.

Alisema alikuwa anafahamu jinsi watu wanavyomshambulia Wema kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kutopata mtoto na amemsifia kwa kuusema ukweli.

Hata hivyo aliwashauri watumiaji wa mtandao ya kijamii kuitumia vyema na sio kuitumia kuwatusi mastaa wao kwakuwa ni kweli maneno yao huwaumiza kama binadamu wengine.

0
Hapa kuna Sifa 13 Watakazozitumia CCM Kumteua Mgombea Urais Kupitia chama Hicho, HEBU ZIONE


Mchakato wa kumpata mgombea urais ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye atabeba jukumu la kupeperusha bendera ya chama hicho ili kukipa ushindi katika Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, sasa tunahesabu siku.
 
Baadhi ya makada wa chama hicho wakiwemo wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), wanasema mchakato huo huenda ukaanza Mei mwaka huu.
 
Akizungumza na Mwandishi wetu, Mjumbe wa NEC kutoka mkoani Arusha ambaye hakutaka jina lake liandikwe, alisema katika uchaguzi wa mwaka huu, CCM kitaandika historia ya kumteua mgombea urais mwenye vigezo vyote.
 
Alisema mgombea huyo ni yule ambaye atakidhi vigezo 13 ili aweze kukivusha chama hicho kiendelee kushika dola si kuteua mgombea anayetokana na shinikizo la makundi ya watu mbalimbali kama ilivyoanza kujionesha kwa baadhi ya wagombea wenye dhamira ya kuwania nafasi hiyo.
 
Mjumbe huyo alikwenda mbali zaidi na kusisitiza kuwa, chama hicho kina utaratibu mzuri wa kuchagua wagombea wake kwenye nafasi ya urais, ubunge na madiwani ambao ndio utazingatiwa katika kuwapata wagombea si vinginevyo.
 
"Chama kikichagua mgombea kwa sababu ya ushabiki na kelele za makundi ya watu kudai mwanachama fulani ndiye anayefaa kuwa rais na kutaka achukue fomu watamuunga mkono, nchi haitakuwa salama na sababu tunazo.
 
"Lazima tujiulize kwanini iwe yeye wakati kuna baadhi ya makada ndani ya CCM wanaotajwa kutaka kuwania urais wakiwa na sifa zinazokubalika ndani ya chama kuliko huyo wanayemtaka...chama hakiwezi kusikiliza maneno ya watu kwani nafasi yenyewe ni nyeti,"alisema.
 
Aliongeza kuwa, uteuzi wa mgombea urais CCM baada ya wagombea wote kuchukua fomu za kuomba kuwania nafasi hiyo, kila mmoja atatakiwa kutafuta wadhamini kwenye mikoa 10 na kuzirudisha kwa mchakato mwingine.
 
Majina ya wagombea hao yatapelekwa kwenye Kamati ya Maadili ambayo itayapitia na baadaye kwenda Kamati Kuu kwa ajili ya uteuzi wa majina matano.
 
"Haya majina matano yatapelekwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ili yaweze kupigiwa kura na kupatikana majina matatu ambayo yatapelekwa katika Mkutano Mkuu ambao nao utapiga kura ili kumpata mgombea mmoja," alisema.
 
Sifa za wagombea urais
Mjumbe huyo aliongeza kuwa, ili mgombea urais wa CCM aweze kuchaguliwa katika nafasi hiyo mbali ya kupitia taratibu alizozitaja awali ndani ya chama:
  
kwanza ; anapaswa kuwa na uwezo wa kuliongoza Taifa kwa kuzingatia uzoefu alionaokatika uongozi wa shughuli za Serikali, umma na taasisi.
 
Pili; awe mwadilifu, mwenye hekima na busara.
 
Tatu; awe na elimu ya kiwango cha Chuo Kikuu au inayolingana na hiyo.
 
nne; awe mwenye upeo na uwezo mkubwa wa kudumisha, kuimarisha na kuendeleza Muungano wetu, umoja, amani na utulivu wetu pamoja na mshikamano wa kitaifa.
 
Tano; awe mtu wa kuona mbali, asiyeyumbishwa, mwenye uwezo wa kufanya uamuzi wa busara kuhusu masuala nyeti na muhimu ya Taifa kwa wakati unaofaa.
 
sita; awe na upeo mkubwa usiotiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifaili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na Dunia yote kwa jumla.
 
Saba; asiwe mtu mwenye hulka ya udikteka au ufashisti bali aheshimu na kuilinda Katiba ya nchi, sheria, utawala bora, kanuni na taratibu za utawala bora.
 
nane; awe mtetezi wa wanyonge, kusimamia haki za binadamu, mzingatiaji makini wa maendeleo ya raia wote na asiwe na tamaa ya kujitafutia umaarufu wake binafsi.
 
Tisa; awe mstari wa mbele kuzifahamu, kuzieleza, kuzitetea na kuzitekeleza Sera za CCM na Ilani ya CCM ya Uchaguzi.
 
kumi; awe mpenda haki na jasiri wa kupambana na dhuluma,maovu yote nchini.
 
kumi na moja; asitumie nafasi yake ya uongozi kujilimbikizia mali.
 
Kumi na mbili; awe ni mtu anayekubalika na wananchi.
  
kumi na tatu; awe makini katika kuzingatia masuala ya uwajibikaji wa uongozi, watendaji, asiyevumilia uzembe katika utekelezaji wa majukumu ili kuinua nidhamu ya kazi, tija na ufanisi. 
 
Aliongeza kuwa, kati ya sifa 13 za mgombea urais CCM zilizotajwa na Mjumbe wa NEC, kutokana na uchanga wanchi yetu, lazima mgombea awe na upeo mkubwa usioatiliwa shaka kuhusu masuala ya kimataifa ili aweze kuwa kiungo imara kati ya nchi yetu na Dunia yote kwa jumla.

0
CCM yapanga Kuing'oa CHADEMA Kwa Chopa Moshi Mjini


CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, kimeanza kulisaka Jimbo la Moshi Mjini kwa kutumia helikopta (chopa) ili kiweze kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu ujao.
 
Katika mkutano wao wa hadhara uliofanyika jana kwenye Viwanja vya Soko la Pasua, Kata ya Bomambuzi, kada wa chama hicho Buni Ramole kwa jina maarufu 'Buni', alitumia usafiri huo kufika eneo la mkutano.
 
Akihutubia mamia ya wanachama wa CCM na wananchi walioshiriki mkutano huo, Ramole alisema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimepoteza sifa ya kuendelea kuliongoza jimbo hilo hivyo kinapaswa kukaa pembeni.
 
Alisema umefika wakati wa CCM kuliongoza jimbo hilo ili kuwaletea wananchi maendeleo baada ya jimbo hilo kushikiliwana mbunge wa CHADEMA kwa vipindi vitatu mfululizo.
 
"Naomba niwaeleze kuwa, jimbo hili kuongozwa na mbunge wa CHADEMA, Bw. Philemon Ndesamburo kwa vipindi vitatumfululizo...katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu lazima lirudi CCM, upinzani hawajafanya kitu zaidi ya kusababisha mateso kwa wananchi, sasa watupishe," alisema.
 
Aliongeza kuwa, mwaka 2010 wakati Bw. Ndesamburo alikupata ridhaa ya wananchi aweze kuliongoza jimbo hilo kwa awamu ya tatu, aliahidi mambo mengi.
 
Mambo hayo ni pamoja na kufungua viwanda vilivyofungwa katika Mji wa Moshi lakini hadi sasa ameshindwa kuitekeleza ahadi hiyo hivyo ni wazi kuwa aliwadanganya wananchi.
 
Kada huyo ambaye pia ni mfanyabiashara, alisema CCM kimejipanga vizuri kuhakikisha kinalichukua jimbo hilo kwa ushindi wa kishindo ambapo moja ya mambo ambayo chama hicho kitafanya baada ya kushinda ni kuwaletea wananchi maendeleo na kufungua viwanda vyote vilivyofungwa.
 
"Jambo lingine ambalo tutalifanya ni kata zote za Mji wa Moshi, kuunganishwa na barabara za viwango vya lami,nitashirikiana na watendaji wa chama changu kuhakikisha tunapata ushindi wa kishindo...tutaendelea kutumia chopana kupita kila kata ili tuweze kuwafikia wananchi wote ili kuwaeleza ahadi zetu," alisema.
 
Akizungumzia hatua ya Bw. Ndesamburo kutangaza kutogombea tena ubunge wa jimbo hilo na nafasi hiyo kumpa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Moshi, Bw. Japhary Michael, alisema inaonesha kuwa CHADEMA hakina demokrasia.
 
"Hivi karibuni Ndesamburo alitangaza kuachia ubunge na kumkabidhi mikoba yake Japhary Michael, hii inaonyesha wazi kuwa chama hicho hakina demokrasia bali ni sawa na SACCOSya mtu anayeweza kuitumia atakavyo," alisema.
 
Ramole ni mmoja wa makada wa CCM ambaye ametangaza nia ya kutaka kuwania ubunge wa jimbo hilo muda ukifika.
 
Mwaka 2010, Ramole alikuwa mmoja kati ya wagombea tisa ndani ya CCM waliojitokeza kuwania ubunge wa jimbo hilo ambapo baada ya kupigiwa kura, alishinda na kushika nafasi ya kwanza akipata kura 1,554.
 
Nafasi ya pili ilishikwa na Bw. Thomas Ngawaiya aliyepata kura 1,539 ambapo Justine Salakana alishika nafasi ya tatubaada ya kupata kura 1,152.
 
Licha ya Ramole kuongoza katika kura ya maoni, jina lake lilienguliwa na chama hicho ambapo Salakana aliyeshika nafasi ya tatu, ndiye aliyepeperusha bendera ya chama hicho kwa tiketi ya CCM lakini hakufurukuta kwa Bw. Ndessamburo.

0
Muasisi wa CCM Zanzibar, Mzee Hassan Nassor Moyo Afukuzwa Uanachama wa Chama Hicho


Mwanasiasa mkongwe na kada wa CCM aliyepata kushika nyadhifa mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwaziri, Mzee Hassan Nassor Moyo amefukuzwa uanachama wa chama hicho ambacho yeye ni mmoja wa waasisi wake, akiwa mwanachama namba 7.
 
Mzee Moyo (81) ni miongoni mwa viongozi waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar pia wa mwaka huo na mara tu baada ya Muungano, aliteuliwa kuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
 
Kufukuzwa kwake kumetajwa kumetokana na kwenda kinyume na maadili ya chama pamoja na matamshi yasiyokubaliana na sera za chama hicho.
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Unguja, Aziza Iddi Mapuri, matamshi mbalimbali ya Moyo aliyokuwa akiyatoa katika mikutano ya hadhara inayofanywa na Chama cha Wananchi (CUF) inaonesha kwamba amekisaliti chama akiwa mzee wa kupigiwa mfano katika CCM.
 
Katika taarifa hiyo, imetoa mfano kuwa Aprili 30, 2014 katika mkutano wa CUF uliofanyika Kibandamaiti ambapo Katibu wa CUF, Seif Sharif Hamad alimsimamisha Mzee Moyo ambaye alisema serikali tatu ndiyo msimamo wa Wazanzibari wote.
 
Aidha, katika mkutano uliofanyika Tibirinzi huko Pemba Februari 9, 2014 Mzee Moyo alijitambulisha kuwa ni mwenyekiti wa maridhiano kutoka CCM ilhali si kweli, kwani Chama cha Mapinduzi hakimtambui kiongozi huyo.
 
Katika taarifa hiyo imesema CCM baada ya kutafakari kwa kina imebaini kiongozi huyo amekuwa akiongoza upotoshaji wa hali ya juu na hafai kuendelea kuwa mwanachama wa chama hicho tawala nchini.
 
Taarifa hiyo iliongeza kuwa, Mzee Moyo wakati akihutubia kongamano la CUF hapo katika ukumbi wa taasisi ya Kiswahili na lugha za kigeni, alibeza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kwamba mkataba wa Muungano wa Aprili 22 haujulikani uliopo na wabunge wa Bunge Maalumu la Katiba walikuwa hawajui wanachokifanya.
 
“Kutokana na matukio yote hayo na matamko anayoyatoa Mzee Moyo amepoteza sifa za kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi ambaye ni mfano wa kutegemewa wa wazee na vijana,” alisema.
 
Akizungumza na mpekuzi kwa njia ya simu kutoka Tanga, Mzee Moyo alisema hajutii uamuzi huo kwa sababu yeye hakuzaliwa kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi daima.
 
“Mimi sijutii kufukuzwa katika Chama Cha Mapinduzi kwa sababu sikuzaliwa kuwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi milele......natofautiana na CCM katika mambo mbali mbali ikiwemo suala la muundo wa muungano,’’ alisema.
 
Katika siku za hivi karibuni Mzee Moyo katika majukwaa ya CUF amekuwa akitamka bayana kwamba muungano wa serikali mbili umepitwa na wakati na Zanzibar ipo haja ya kuwa na mamlaka kamili.
 
Mbali ya uwaziri wa Katiba na Sheria katika Serikali ya awamu ya kwanza, nyadhifa nyingine alizotumikia Mzee Moyo katika serikali ya Muungano ni pamoja na mbunge kwa muda mrefu na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
 
Kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameshika nyadhifa mbalimbali tangu mwaka 1964 na kufanya kazi kwa karibu sana na Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume kwa kuongoza Wizara ya Kilimo kwa muda mrefu akifanya kazi kubwa ya kutekeleza ilani ya ASP ya kugawa ardhi kwa wananchi wote.
 
Ni kiongozi wa mwanzo kuwa mwanachama wa CCM ilipozaliwa mwaka 1977 baada ya TANU kuungana na ASP ambapo katika sherehe zilizofanyika katika Uwanja wa Amaan, Zanzibar, alikabidhiwa kadi namba 7.
 
Akizungumzia suala hilo, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Nape Nnauye alisema CCM mkoa wa Magharibi ina uwezo wa kumvua uanachama, hivyo kilichofanyika kwa mujibu wa Katiba ya CCM ni sahihi.
 
Alifafanua kuwa, kwa wanachama wa kawaida, hatua za kinidhamu zinaweza kuchukuliwa katika ngazi za chini, bali hali ni tofauti kwa viongozi akitolea mfano diwani, mbunge au mwakilishi ambao maamuzi ya kuwachukulia hatua za kinidhamu yanapaswa kufanywa na vikao vya juu.
 
“Kwa hiyo ndugu yangu, Halmashauri ya chama ya mkoa ina mamlaka ya kumvua uanachama mwanachama wake wa kawaida, hivyo kilichofanyika kwa Mzee Moyo ni sahihi kwa mujibu wa Katiba…kitakachokuja kwetu ni taarifa.
 
“Lakini mengineyo, kama kwanini amechukuliwa hatua… watu wa mkoa wa Magharibi wenyewe ndio wanaweza kueleza zaidi, sisi ni watu wa kupokea taarifa kwa kuwa Katiba inawapa nguvu ya kufanya maamuzi ya kinidhamu,” alisema Nnauye.